Chama cha Hakimiliki na Hakishiriki (COSOTA) leo kimekabidhiwa rasmi kwa uongozi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara kilipokuwa awali.
Hafla ya makabidhiano ya Chama hicho imefanyika jijini Dar es Salaam baina ya Makatibu Wakuu wa Wizara hizo mbili na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa tasnia ya sanaa wakiwemo viongozi wa taasisi za Serikali, wasanii wa muziki, filamu, sanaa za maonesho na waandishi wa vitabu pamoja na miswada na wengineo.
Katika hafla hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi alisema kuwa tukio hilo ni matunda ya uamuzi makini wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli uliofanywa kwa wakati muafaka ambapo nchi yetu imeingia kwenye uchumi wa kipato cha kati.
“Tunamshukuru Rais Magufuli kwa kufanya uamuzi mgumu wenye manufaa kwa wasanii wa Tanzania kwa kuwa anatambua sanaa ina umuhimu mkubwa katika maisha ya binadamu hivyo wasanii wetu hawapaswi kuwa maskini,” alisema Dkt. Abbasi.
Pia Dkt. Abbasi alieleza kuwa uamuzi wa kuihamisha COSOTA ulitekelezwa ndani ya saa 24 baada ya tamko la Rais Magufuli alilolitoa Julai 12 mwaka huu akiwa Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma na yeye kuahidi kuwa ataendelea na kanuni hiyo ya saa 24 za maajabu ya kiutendaji.
“Nawaahidi kuwa ndani ya saa 24 zijazo kuanzia muda huu mambo mawili yatatokea, kwanza nitakutana na Bodi ya COSOTA na kusikiliza mipango yao katika kutekeleza kivitendo COSOTA mpya yenye kupigania haki za wasanii, pili ndani ya saa 24 hizi nitakutana na menejimenti na wafanyakazi wote wa COSOTA kuona tena mikakati yao ya kumfanya msanii awe tajiri kwa kunufaika na kazi zake”, alieleza Dkt. Abbasi.
Aidha kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Prof. Riziki Shemdoe alibainisha kuwa COSOTA ni taasisi muhimu katika kutunza na kulinda maslahi ya wasanii hivyo wizara yake itaendelea kutoa ushirikiano kwa chama hicho muda wowote itakapohitajika kwa ajili ya maendeleo ya wasanii na taifa kwa ujumla.
Naye Mtendaji Mkuu wa COSOTA, Bi. Doreen Sinare alieleza kuwa wanajivunia uongozi makini wa Rais. Dkt. John Pombe Magufuli kwani ndani ya miaka mitano ya uongozi wake chama hicho kimepata mafanikio makubwa ikiwemo kuanzishwa kwa Bodi ya COSOTA pamoja na kuhamishiwa kwenye wizara inayohusika na wadau wa sanaa.
“Tunaahidi kuendeleza mazuri yote tuliyotoka nayo Wizara ya Viwanda na tunatarajia Wizara ya Habari itatupatia ushirikiano zaidi ili kuendelea kusukuma gurudumu la maendeleo kwa wasanii wa Tanzania,” alisema Doreen.
Chama cha Hakimiliki na Hakishiriki (COSOTA) kiliundwa mwaka 1999 kupitia Sheria namba 7 ya Hakimiliki na Hakishiriki (The Copyrights na Neighbouring Rights Act).
Hakimiliki ©2023 Habari - MAELEZO