TAARIFA KWA UMMA
Serikali Yafafanua Mawaziri Kuzungumza, Yaendelea Kueleza Utekelezaji Ripoti Ya Cag Sekta Za Kilimo Na Mifugo
Dodoma, April 16, 2018:
Serikali imeendelea kueleza hatua za utekelezaji wa hoja za ukaguzi zilizoainishwa katika Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2016/17 kwa kuainisha hatua mbalimbali zilizochukuliwa katika Sekta za Kilimo na Mifugo huku ikifafanua misingi ya kikatiba na kisheria kwa mawaziri kujitokeza kufanya hivyo.
Dkt. Mwakyembe:Mawaziri Hawavunji Sheria
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe akiongea na waandishi wa habari Leo Mjini Dodoma na kufafanua kuwa kitendo cha mawaziri kueleza utekeleza wa hoja za ukaguzi ni utamaduni mpya wa kiuwajibikaji unaoletwa na Serikali ya Awamu ya Tano
Kabla ya ufafanuzi kuhusu utekelezaji katika sekta za kilimo na mifugo, Dkt. Harrison Mwakyembe, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia kitaaluma ni mwanasheria aliyebobea katika masuala ya Katiba, amefafanua kuwa kitendo cha mawaziri kueleza utekelezaji wa hoja za ukaguzi ni utamaduni mpya wa kiuwajibikaji wa Serikali ya Awamu ya Tano na itachukua muda kuzoeleka lakini amewahakikishia Watanzania kuwa hakuna sheria yoyote ya nchi wala ya kimataifa iliyovunjwa.
Akieleza msingi wa kikatiba na kisheria wa hatua hiyo, Dkt. Mwakyembe aliitaja ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa pamoja na kutoa uhuru wa kupashana habari, Serikali inapewa wajibu wa kutoa taarifa kuhusu utekelezaji. Aliongeza zaidi kuwa misingi hiyo ya kikatiba imepambanuliwa zaidi katika Sheria ya Haki ya Kupata Taarifa na. 6 ya mwaka 2016.
“Hakuna sheria yoyote duniani sembuse hapa nchini inayoizuia Serikali kueleza utekelezaji ilioufanya katika jambo lolote lenye manufaa kwa umma. Kama yupo mwenye hicho kifungu kinachotuzuia mawaziri kueleza utekelezaji katika sekta zetu atuoneshe. Nashawishika tu kusema wanaoumizwa na hatua hii ni wale wasiotaka kusikia changamoto zinazowarudisha nyuma wananchi zikitatuliwa,” alisema.
Akiichambua Sheria ya Ukaguzi wa Umma ya Mwaka 2008 (na mabadiliko ya mwaka 2013), Dkt. Mwakyembe alikitaja kifungu cha 38(1)-(3) kuwa zinaainisha hatua mbalimbali za kibunge kuhusu ripoti ya CAG pamoja na majibu ya Serikali yaliyoandaliwa na Maafisa Masuuli na kwa kuwa kuanzia hapo ripoti zote huwa wazi kwa umma si mawaziri tu bali hata wananchi wanaruhusiwa kuzisoma na kuzijadili.
Dkt. Tizeba: CAG ametuonesha njia
Waziri wa Kilimo, Dkt. Charles Tizeba akiongea na waandishi wa habari Leo Mjini Dodoma ambapo alisema Kufuatia Taarifa ya CAG Wizara imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kufanya ukaguzi wa kustukiza ili kubaini madawa feki lakini pia ilifika hatua wataalamu wa kilimo kutoka Wizarani na taasisi nyingine wapatao 200 wakapelekwa maeneo mbalimbali nchini kutoa elimu sahihi ya kukabiliana na visumbufu mimea.
Akizungumzia Sekta ya Kilimo, Dkt. Tizeba alisema sehemu kubwa ya ripoti ya CAG imegusa kwa usahihi changamoto mbalimbali katika udhibiti wa visumbufu vya mimea ambavyo hujumuisha pia wadudu wanaoshambulia mazao mbalimbali.
Alisema, tangu ukaguzi ulipobaini changamoto hizo Juni mwaka jana, Wizara imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kufanya ukaguzi wa kustukiza ili kubaini madawa feki lakini pia ilifika hatua wataalamu wa kilimo kutoka Wizarani na taasisi nyingine wapatao 200 wakapelekwa maeneo mbalimbali nchini kutoa elimu sahihi ya kukabiliana na visumbufu mimea.
Waziri Tizeba amesisitiza kuwa, mbali na hatua hizo, Wizara imeunda timu ya wataalamu kuchambua kila eneo lililobainishwa kuwa na mapungufu ili kuyatafutia ufumbuzi wa kudumu.
Imetolewa na:
Dkt. Hassan Abbasi,
Mkurugenzi, Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali.
Hakimiliki ©2023 Habari - MAELEZO