Dar es Salaam, Februari 7, 2018:
Wakati ripoti na takwimu mbalimbali za kimataifa zikiitaja Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazofanya vyema katika nyanja za uchumi na utawala bora, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi thabiti wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, imeendelea kutafsiri takwimu hizo kivitendo kwa kuendeleza kwa kasi utekelezaji wa miradi mbalimbali.
Katika taarifa ya mwezi Januari, 2018 iliyotolewa leo Dar es Salaam, ikiwa ni mkakati mpya wa Serikali kuwapatia wananchi mrejesho wa utekelezaji, hatua kubwa zinaendelea kufikiwa katika sekta mbalimbali za kijamii.
Tanzania Kinara Afrika, Duniani
Katika kipindi hiki, ripoti mbalimbali za taasisi za kimataifa zimeonesha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi chache za Afrika na Dunia ambazo zinafanya vizuri katika uchumi na maendeleo. Ripoti ya World Economic Forum (WEF) ya Januari 23, 2018 iitwayo “The Inclusive Development Index,2018,” imeitaja Tanzania kuwa ya pili Afrika na ya kwanza Kusini mwa Jangwa la Sahara katika uchumi jumuishi kwa maana ya uchumi unaogusa maisha ya watu wake.
Katika muktadha wa ukuaji uchumi, ripoti za FORESIGHT AFRICA iitwayo “Top Priorities for the Continent in 2018” na Benki ya Dunia (WB) iitwayo “Global Economic Prospects-Broad-Based Upturn, but for How Long?” Tanzania imetajwa kuwa katika nchi 5 Bora za Afrika katika ukuaji wa uchumi. Nchi nyingine ni Ghana, Ethiopia, Kodivaa na Senegali.
Aidha, katika mawanda ya Utawala Bora; kigezo muhimu katika kuchagiza maendeleo ya uchumi na ustawi wa jamii, Orodha ya Hali ya Demokrasia Duniani (2017 Democracy Index) ya jarida mashuhuri duniani la The Economist iliyozinduliwa Februari 2, 2018, imeonesha Tanzania inafanya vizuri ikiwa ya kwanza katika Afrika Mashariki.
Serikali imezipokea takwimu na ripoti hizi kama chachu ya kuwakumbusha viongozi na watendaji wote kuwa kazi ya kuwahudumia wananchi wetu inatambulika na hivyo inapaswa kuendelea kwa kasi kama utekelezaji wa baadhi ya miradi unavyoonesha hapa chini.
Bajeti Yaondoa Maumivu Sekta ya Afya
Katika mwaka huu wa fedha Serikali ilifanya uamuzi wa kihistoria wa kupandisha Bajeti kutoka wastani wa Bilioni 30 mwaka 2015 hadi Bilioni 269 ikiwa ni jitihada za kuwaondolea wananchi maumivu ya kukosa tiba muhimu.
Kufikia Januari, 2018 mageuzi makubwa yamefanyika katika hospitali na vituo vya afya nchini kwa kununuliwa vifaa vilivyokuwa vinawapa usumbufu sana wananchi. Katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, mashine mpya zikiwemo, CT-Scan zenye uwezo mkubwa zimenunuliwa ambapo sasa wastani wa wagonjwa wanaopimwa imepanda kutoka 20 hadi 50 kwa siku. Mashine za kisasa kama CT-Scan na MRI na vifaa vya kisasa vya tiba ya mionzi ya saratani pia vimenunuliwa katika hospitali za Ocean Road, Benjamin Mkapa-Dodoma na Bugando.
Aidha, Serikali imenunua vifaa tiba vingi vinavyosaidia Tanzania kutoa huduma za juu za kibingwa, huduma ambazo miaka michache iliyopita Watanzania wengi walilazimika kutafuta fedha nyingi kwenda nje ya nchi kutibiwa. Katika eneo la tiba ya figo Hospitali ya Taifa Muhimbili imeshafanya upandikizaji wa kwanza na wa kihistoria wa figo huku wagonjwa wanaohudumiwa kwa siku huduma za kawaida za figo wakiongezeka kutoka 68 hadi 126 kutokana na mashine mpya 25 zilizonunuliwa.
Aidha, ukiacha Kituo cha Tiba ya Moyo cha Jakaya Kikwete ambako vifaa vya kisasa vimeifanya Tanzania kuanza kuwa kimbilio la nchi nyingi za Afrika kuacha kwenda Ulaya na India na kuja kupata tiba, nchi yetu pia imekuwa ya kwanza Afrika Mashariki kwa hospitali ya umma ya Muhimbili kufanya oparesheni ya kuwawekea watoto vifaa vya kuwawezesha kusikia (Cochlear Implants). Huduma hii hapa nchini imepunguza gharama kwa asilimia hadi 60.
Katika kipindi hiki pia, Bohari ya Dawa (MSD) nayo imeleta mabadiliko katika maisha ya watanzania. MSD imetatua tatizo la miaka mingi la dawa na vifaa muhimu kutopatikana katika vituo vya afya na hospitali. Ununuzi wa moja kwa moja kwa wazalishaji wa dawa na vifaa na ufuatiliaji makini vimepunguza bei ya dawa kwa asilimia 40 na pia upatikanaji wa dawa kwa sasa ni asilimia 80 hadi 95.
Miradi ya Maji Yaleta Matumaini
Sekta ya maji ni moja ya eneo ambalo ukweli wa kazi za Serikali ya Awamu ya Tano unaonekana kivitendo kuanzia mijini hadi vijijini ambako miradi mbalimbali inaendelea kutekelezwa. Itakumbukwa kuwa lengo la Serikali kufikia mwaka 2020 ni kufikisha huduma ya maji kwa asilimia 85 vijijini kutoka asilimia 67.7 mwaka 2015; makao makuu ya mikoa asilimia 95; Dar asilimia 95 na miji mikuu ya wilaya asilimia 90.
Miradi ya mabilioni ya shilingi inatekelezwa kote nchini hivi sasa na ipo ambayo tayari imeshakamilika na wananchi wameanza kupata maji. Hadi sasa kwa ujumla takribani miradi 1,423 imekamilika na kuna vituo vya maji 117,190 vyenye uwezo wa kuhudumia wastani watanzania milioni 29 sawa na asilimia 79. Kati ya miradi hiyo, miradi 388 imekamilika ndani ya miaka hii miwili. Serikali pia imesajili Kamati za Maji 2,285 kwa ajili ya kuwawezesha wananchi kuisimamia miradi iliyoko katika maeneo yao ijiendeshe kwa ufanisi.
Umeme Vijijini Wayaangaza Maisha
Tulieleza katika ripoti ya Januari mwaka huu hatua mbalimbali ambazo Serikali imezichukua kuhakikisha uzalishaji wa umeme wa kihistoria nchini. Katika usambazaji wa umeme mijini na vijijini kazi imeendelea kwa kasi kila mkoa nchini ikiwa ni utekelezaji wa Mradi wa REA Awamu ya Tatu.
Katika awamu hii Serikali itatumia na imeshaanza kutumia Bilioni 985.9 kuwafikia wananchi katika vijiji 3,559 katika mikoa 25 nchini. Aidha, Usambazaji wa umeme katika awamu hii utatoa kipaumbele kwa sekta muhimu kama vile shule, zahanati, vituo vya afya na hospitali.
Barabara, Njia za Juu Zaja
Katika sekta ya miundombinu ya barabara, wakati miradi ya mabilioni ikiendelea huku ujenzi kwa kiwango cha lami ukiendelea sehemu mbalimbali nchini kukamilisha kazi ya kuiunganisha mikoa na miji muhimu kwenda barabara kuu za kitaifa, Serikali imeanzisha Wakala wa Barabara za Miji na Vijiji (TARURA) ili kufikisha huduma zaidi vijijini.
Ujenzi wa barabara pia unakwenda sambamba na azma ya Serikali kutatua kero mbalimbali za foleni hasa katika jiji la kibiashara la Dar es Salaam. Tayari ujenzi wa barabara ya juu TAZARA umefikia asilimia 70 kukamilika huku ujenzi eneo la Ubungo ukiwa umeshazinduliwa.
Katika kipindi kifupi kijacho ujenzi wa barabara za juu utaanza kutokana na hatua za usanifu kuanza katika makutano ya barabara maeneo ya Chang’ombe, Uhasibu, Kamata, Moroco, Mwenge, Magomeni na Tabata, Dar es Salaam. Ni matarajio ya Serikali kuwa kazi za usanifu na upembuzi zitakamilika kufikia Juni, 2018 ili miradi hii ianze kutekelezwa mwaka huu.
Soko la Bidhaa Kuwainua Wakulima
Katika sekta ya kilimo, mbali na hatua kubwa zilizochukuliwa ikiwemo kuongeza maafisa ugani kutoka 9,558 mwaka 2015 hadi 13,532 mwaka 2017, vituo vya mafunzo ya kilimo na uvuvi vya Kata kuongezeka kutoka 147 mwaka 2015 hadi 322 mwaka jana na usambazaji wa mbolea kuendelea kwa kasi, mwaka huu Serikali itaanzisha mfumo mwingine muhimu katika kuwakomboa wakulima.
Wakati wowote kuanzia sasa soko la kimataifa la mazao ya kilimo litaanza ikiwa ni kituo muhimu cha kuwaleta wanunuzi wote wa mazao yaliyohifadhiwa kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani kutoka ndani na nje ya nchi washindanishwe ili kupatikana bei nzuri kwa wakulima.
Madeni ya Wafanyakazi Tayari?
Katika mkutano wa leo na wanahabari pia walitaka kujua iwapo ahadi ya Mhe. Rais Magufuli ya kutoa fedha kwa ajili ya madeni mwezi huu imetekelezwa? Napenda kuwapa habari njema watoa huduma mbalimbali na watumishi wa Serikali kuwa tayari fedha hizi zipo na zitaanza kutolewa wakati wowote mwezi huu kupitia wizara husika kutokana na ukaguzi wa madeni uliokuwa ukifanyika kuendelea kukamilika.
Katika taarifa ijayo tutaendelea kufafanua utekelezaji wa kazi zinazoendelea kwa kasi katika sekta nyingine na ahadi mbalimbali za Serikali. Natumia fursa hii kuwahakikishia wananchi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ina nia, dhamira na imejipanga kuondoa kero mbalimbali zinazowakabili wananchi. Ni vyema kila mwananchi akaungana na safari hii ya mabadiliko ya kweli kwa kujituma kufanya kazi, kulipa kodi na kuwa mzalendo.
Kwa maelezo zaidi kuhusu taarifa ya leo ikiwemo picha za miradi zinazoambatana na taarifa hii tafadhali tembelea:
Tovuti: www.maelezo.go.tz
Blogu: www.blog.maelezo.go.tz
Twitter: TZ_MsemajiMkuu
Imetolewa na:
Dkt. Hassan Abbasi
Mkurugenzi, Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali.
Hakimiliki ©2023 Habari - MAELEZO