Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli aongoza Mamia ya Wakazi wa Chato katika Mazishi ya Dada yake Marehemu Monica Magufuli yaliyofanyika Chato Mkoani Geita.Agosti 21,2018
Dada wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aitwaye Monica Joseph Magufuli aliyefariki dunia Jumapili tarehe 19 Agosti, 2018 katika hospitali ya Bugando Jijini Mwanza amezikwa leo katika makaburi ya familia yaliyopo katika kijiji cha Mlimani, Wilaya ya Chato Mkoani Geita.
Misa Takatifu ya Mazishi ya Monica Joseph Magufuli imeongozwa na Askofu Jimbo Katoliki la Rulenge Mhashamu Severine Niwemugizi aliyeambatana na Maaskofu wengine saba, pia imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Marais Wastaafu Mhe. Ali Hassan Mwinyi, Mhe. Benjamin William Mkapa na Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.
Viongozi wengine waliohudhuria mazishi hayo ni Waziri Mkuu Mstaafu wa Kenya Mhe. Raila Amolo Odinga, Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara Ndg. Philip Mangula, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, Mawaziri, Wabunge, Viongozi Wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama, Viongozi wa Madhehebu ya Dini, Viongozi wa vyama vya siasa na viongozi wengine mbalimbali wa Mikoa, Wilaya, Taasisi, Idara na Kampuni.
Katika salamu zake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewashukuru viongozi na wananchi wote walijitokeza kuungana na familia katika kumsindikiza Dada yake katika safari yake ya mwisho na amesema familia inatambua upendo, heshima na mshikamano mkubwa ambao wameuonesha kwao. “Mmetuonesha upendo mkubwa sana na kweli ujio wenu na kuungana nasi katika tukio hili mmetufariji sana, asante sana kwa upendo huu na Mungu awabariki sana” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Hakimiliki ©2023 Habari - MAELEZO