Na Paschal Dotto-MAELEZO
13-07-2019
Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni ametembelea nchini kwa Ziara binafsi ya siku moja na kupokelewa na Mwenyeji wake Rais wa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Pombe Magufuli katika uwanja wa ndege Chato Mkoani Geita.
Akizungumza katika hafla ya kumkaribisha, Rais Magufuli amempongeza Rais wa Uganda pamoja na raia wa Uganda kwa kuendelea kudumisha uhusiano ulioachwa na Baba wa taifa Mwl.Julius Kambarage Nyerere kwani sasa uhusiano umeendelea kudumisha uchumi kati ya nchi hizi mbili.
“Uhusiano huu ulikuwepo tokea tawala za Baganda(Uganda) na Karagwe (Tanzania), lakini na wakati wa ukoloni hususani baada ya vita ya pili ya dunia nchini hizi mbili zilitawaliwa na Uingereza kwa hiyo undugu wetu ni wa kweli, lakini kutoka na uhusiano huu nchi zetu zinafaidika kiuchumi mfano biashara kati ya Tanzania na Uganda mwaka 2018 zilifikia shilingi Bilioni 358.697 kutoka bilioni 178.191 mwaka 2015 hii inadhihirisha kuna mahusiano mazuri kwetu”, Alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli alisema kuwa katika kuendeleza uchumi na mahusiano kati ya nchi hizo mbili Uganda wana miradi 22 ambayo wamewekeza nchini Tanzania yenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 143.25 ambayo imetoa ajira kwa watanzania 2,230.
Kwa upande wa usafirishaji Rais Magufuli alisema kuwa, wafanyabiashara kutoka Uganda wanapitisha mizingo yao nchini kwa kutumia bandari ya Dar es Salaam huku mwaka jana wakipitisha zaidi ya tani 188,591 na kumhakikishia Rais Museveni kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na wafanyabiashara kutoka Uganda ili kuongeza usafirishaji mizigo kupitia bandari ya Dar es salaam.
“Tumeshafanya Ukarabati wa Reli yetu ya kati kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza, tumefufua meli ya kubeba mizigo ya kutoka Mwanza kwenda Uganda, kwa hiyo kwa wafanyabiashara kutoka Uganda kwa sasa unaweza ukapakia mizigo ukapeleka moja kwa moja mpaka bandari ya Dar es Salaam na bahati nzuri njia hii ni fupi na mbadala, kwa hiyo nachomekea hilo Mh.Rais ukawaeleze wafanyabiashara watumie njia hii ni fupi”, Alisema Rais Magufuli.
Aidha Rais Magufuli alisema kuwa kwa sasa njia ya kutoka Dar es Salaam mpaka Mwanza ni nzuri kwa wafanyabiashara wanaotumia bandari ya Dar es Salaam kwani Serikali ya Tanzania imeondoa vikwazo ikiwemo kupunguza baadhi ya vituo vya kukagua mizigo.
Rais Magufuli aliongeza kuwa Serikali imeanza ukarabati wa meli ili kumiarisha sekta ya usafirishaji nchini na kurahisisha ufanyaji wa biashara kwa wananchi pamoja na nchini jirani ikwemo Uganda pamoja na nchi zingine kwenye ukanda wa maziwa Makuu.
“Tumetenga zaidi ya Biloni 152 kwa ukarabati wa meli tano na kununua meli mpya kubwa, meli hii haiwezi ikazunguka tuu Mwanza, meli hii katika kujenga uchumi wa nchi tatu na bahati nzuri Uganda mna asilimia 49 ya ziwa vicktoria, Tanzania aslimia 51 na Kenya asilimia 5, kwa hiyo meli hii itazunguka Mwanza, Bukoba, Kisumu na Uganda ili Watanzania, Waganda na Wakenya waweze kufanya biashara na kukuza uchumi wao ”, Alisisitiza Rais Magufuli.
Pia Rais Magufuli amemshukuru Rais Museveni kwa mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima-Uganda mpaka Tanga –Tanzania ambalo litagharimu Dola za Kimarekani bilioni 3.5 lenye urefu wa kilometa 1,440, ambalo litapita Mikoa nane, Wilaya 24 na vijiji 136 hapa Tanzania.
Rais Magufuli alisema kuwa Tanzania na Uganda zitaendelea kushirikiana katika sekta ya utalii kwani mpaka sasa Tanzania imeendelea kuimarisha ukanda wa utalii Kanda ya Ziwa kwa kuzindua mbuga za wanyama za Burigi-Chato ambayo kwa sasa ni hifadhi ya tatu kwa ukubwa ikitanguliwa na Serengeti na Ruaha, pamoja na Lumanika ambayo itazinduliwa hivi karibuni.
Rais aliongeza kuwa ukijumlisha mbuga hizo na mbuga zilizoko Uganda, Kenya na Rwanda sekta ya utalii itaendelea kuimarika zaidi na kuweza kuingiza watalii wengi kwani kwa sasa Tanzania inapokea watalii milioni 1.2, Uganda milioni 1.4 na Kenya milioni mbili huku Misri ikipokea watalii milioni 12 na ikifuatiwa na Morocco miloni 10, kwa hiyo Juhudi za kuanzisha mbuga hizo zitaimarisha sekta ya utalii na ushirikiano baina ya Tanzania na Uganda.
Kwa upande wake Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni alisema kuwa uhusiano kati ya Tanzania na Uganda ni muhimu katika historia kwani ndiyo nchi iliyoisaidia Uganda kupata amani, kwa juhudi za Baba wa Taifa Mwl. Nyerere.
“Nchi za Afrika zilipatwa na changamoto baada ya uhuru, kwani nchi 20 zilikuwa bado hazijapata uhuru, Mwl.Nyerere na Mzee Kaunda walifanya jitihada kubwa ya kuziongoza nchi za kusini mwa Afrika kupata uhuru, Tanzania ilikuwa Maka ya wapigania uhuru, kama waislamu wanakwenda maka sisi wapigania uhuru tunaenda Dar es Salaam kwa hiyo nikija hapa Tanzania nimekuja Hija”, Rais wa Mseveni.
Aidha Rais Museveni alisema kuwa maendeleo ni kutengeneza vitu ambavyo vinawanufaisha wote kama Barabara ili watu wote wapate kuvutumia na kurahisisha maisha yao, alisema pia bomba la mafuta linapita kwa wananchi wa Chato Mkoani Geita kwa hiyo wananchi wataanza kunufaika na mradi huo.
Pia Rais Museveni alimpongeza Rais Magufuli kwa kujenga Reli ya Kisasa kutoka Dar es Salaam mpaka Mwanza kwa awamu ambapo awamu ya kwanza kutoka Morogoro itakamilika hivi karibuni na kuwasaidia watanzania katika usafiri na usafirishaji.
“Nampongeza Rais Magufuli kwa kujenga Reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam Mpaka Mwanza, Reli hii ikikamilika sisi Uganda tutapata Urahisi wa kusafirisha mizigo yetu na bidhaa zetu mbalimbali kutoka katika Bandari ya Dar es Salaam kupitia Mwanza”, Alisema Rais Mseveni.
Rais Museveni alimpongeza pia kwa kujenga Uwanja wa Ndege Chato-Geita kwani maendeleo hayo watayatumia waganda kusafirisha bidhaa na malighafi zao kwa kufanya biashara na watanzania na kudumisha uhusiano ambao uliasisiwa muda mrefu na Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere.
Hakimiliki ©2023 Habari - MAELEZO