Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameagiza kusimamishwa kazi mara moja kwa aliyekuwa Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) katika Mkoa wa Morogoro Mhandisi Godwin Andalwisye na wahandisi wake 12 waliokuwa na jukumu la uangalizi wa barabara katika Mkoa huo.
Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo tarehe 16 Machi, 2020 baada ya kutembelea eneo la daraja la Kiegeya lililosombwa na maji ya mvua tarehe 02 Machi, 2020 na kusababisha kukatika kwa mawasiliano ya barabara ya Dodoma – Morogoro ambayo ni kiunganishi muhimu cha Mikoa ya Kanda ya Kati, Kanda ya Magharibi, Kanda ya Kaskazini Magharibi na nchi jirani za Uganda, Rwanda, Burundi na DRC ambazo husafirisha mizigo na abiria kwenda Dar es Salaam.
Mawasiliano ya barabara hiyo yalirejea baada ya siku 2 na mpaka sasa eneo hilo linapitika kwa madaraja ya muda huku kazi ya kuimarisha ikiendelea.
Mhe. Rais Magufuli ameagiza kusimamishwa kazi kwa Maafisa hao wa TANROADS pamoja na kuwachunguza kama kuna vitendo vya hujuma walivifanya, kutokana na kutochukua tahadhari za kitaalamu za kuzuia maji ya mvua yasisombe daraja lililokuwepo na pia kushindwa kurejesha mawasiliano ya barabara kwa kujenga daraja haraka licha ya fedha za kufanyia kazi hizo kuwepo.
Katika mahojiano na Mkurugenzi wa Matengenezo wa TANROADS Mhandisi Mohamed Ntunda, Mhe. Rais Magufuli ameelezwa kuwa hadi daraja la Kiengeya linasombwa na maji ya mvua, TANROADS katika Mkoa wa Morogoro walikuwa na zaidi ya shilingi Bilioni 3 za matengenezo ya dharura ya barabara.
Akiwa katika eneo hilo Mhe. Rais Magufuli ameliona daraja la muda lililojengwa na Wataalamu wa TANROADS na pia ametembea kwa miguu kuelekea mto unakotirisha maji yake ambapo ameshauri wataalamu hao waangalie uwezekano wa kujenga daraja katika eneo jingine lenye umbali mfupi wa daraja na miinuko inayofaa endapo wataona inafaa kufanya hivyo.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amemuonya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Aloyce Kamwelwe, Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi Patrick Mfugale na Mkurugenzi wa Matengenezo wa TANROADS Mhandisi Mohamed Ntunda kutokana na kutoridhishwa na juhudi zilizofanywa kurejesha mawasiliano ya uhakika katika eneo hilo na ametaka kosa hilo lisirudie.
Ametoa siku 7 kwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano pamoja na TANROADS kuhakikisha eneo hilo linakuwa na daraja la uhakika la kupita magari kama ilivyokuwa kabla ya daraja kusombwa na maji ili kutoathiri shughuli za kiuchumi na kijamii kutokana na kukatika kwa mawasiliano ya barabara.
Mhe. Rais Magufuli amewataka Mameneja wa TANROADS wa Mikoa yote hapa nchini kuhakikisha mawasiliano ya barabara kuu katika Mikoa yao hayakatiki vinginevyo meneja husika atavuliwa wadhifa wake.
Wasafiri na wananchi waliokusanyika katika eneo hilo wakati Mhe. Rais Magufuli akikagua eneo hilo wamelalamikia kukatika kwa mawasiliano ya barabara ya kuelekea Hospitali ya Misheni ya Berega kutokana na kusombwa kwa daraja, hivyo amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Loatha Sanare kuhakikisha Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) inajenga daraja hilo ndani ya siku 7 ili wananchi waendelee kupata huduma za matibabu kama kawaida.
Halikadhalika wananchi hao wamelalamikia kutokamilika kwa ujenzi wa chumba cha upasuaji katika Kituo cha Afya Magubike na Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kuhakikisha jengo hilo linajengwa ndani ya miezi 2.
Pia, Wananchi hao wamelalamikia kuchangishwa shilingi 20,000 kwa kila kaya kwa ajili ya kujenga jengo la maabara katika shule yao ya Sekondari, lakini fedha hizo hazijulikani zilikokwenda na badala yake wameanza kuchangishwa fedha nyingine shilingi 5,000 kwa kila kaya, na Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro Wilbroad Mutafungwa kufuatilia na kuchukua hatua stahiki. Mhe. Rais Magufuli amechangia shilingi Milioni 5 na ameagiza wananchi wasichangishwe fedha za ujenzi wa maabara hiyo.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Morogoro
16 Machi, 2020
Hakimiliki ©2023 Habari - MAELEZO