Na: Lilian Lundo - MAELEZO, Dodoma
Rais Dkt. John Pombe Magufuli amevitaka vyombo vya Dola kuwatafuta na Kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria wahusika waliohujumu kiasi cha shilingi bilioni 2 katika mradi wa maji wa Ntomoko ulioko wilayani Kondoa.
Rais Magufuli ameyasema hayo leo wilayani Kondoa alipokuwa akifungua barabara ya Dodoma hadi Babati yenye kilomita 251.
"Wahusika watafutwe ili warudishe fedha walizochukua au wahakikishe mradi unakamilika. Ni lazima watu waogope mali ya watu masikini," alisema Rais Magufuli.
Ameendelea kwa kusema, kama viongozi wanawajibu wa kuchukua hatua hata kama zinauma lakini ni kwa manufaa ya Watanzania milioni 55.
Wakati huo huo, Rais Magufuli amewataka wananchi wa wilaya ya Kondoa kuitunza miundo mbinu ya barabara ambayo ameizindua. Aidha amesema wapo Wananchi ambao wamekuwa wakiondoa alama za barabarani na kwenda kutengenezea tela za ng'ombe au kujengea vyoo.
Aidha kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amesema barabara hiyo ni muhimum kwani inaunganisha mikoa ya Dodoma na Manyara, vile vile inarahisisha usafiri baina ya nchi za Kusini mwa Afrika na Kaskazini.
Vile vile amesema barabara hiyo itakuwa kichocheo kikubwa cha kukuza utalii, biashara na viwanda kupitia nchi zinapitiwa na barabara hiyo ambazo ni Afrika Kusini, Botswana, Zimbabwe Zambia, Kenya, Ethiopia, Sudan Misri na Tanzania yenyewe kupita Tunduma, Mbeya, Iringa, Dodoma, Arusha hadi Namanga.
Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 251 imegharimu shilingi za Kitanzania bilioni 378.423 fedha ambapo Serikali ya Tanzania imetoa shilingi bilioni 107.654 na fedha zilizobaki zimetolewa na Benki ya Maendeleo ya Afrika na Ubalozi wa Japani hapa nchini.
Mwisho.
Hakimiliki ©2023 Habari - MAELEZO