Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametoa wiki moja kuanzia leo tarehe 19 Machi, 2018 kwa Mawaziri kufanyia kazi na changamoto na maoni yaliyotolewa na wafanyabiashara katika mkutano wa 11 wa Baraza la Taifa la Biashara uliofanyika leo Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Rais Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa baraza hilo ametoa maagizo hayo wakati akihitimisha mkutano huo ambao wafanyabiashara na wawekezaji kutoka sekta mbalimbali wamepata nafasi ya kueleza maendeleo ya shughuli zao, changamoto zinazowakabili na mapendekezo ya kuimarisha biashara na uwekezaji hapa nchini.
Miongoni mwa changamoto hizo ni utozaji wa kodi unaoathiri biashara na uwekezaji, urasimu wa taasisi za Serikali, udhibiti wa bidhaa za kutoka nje ya nchi zinazoathiri uzalishaji wa bidhaa za ndani, uwepo wa sheria na kanuni kandamizi kwa biashara na uwekezaji na utendaji usioridhisha kwa baadhi ya maafisa wa Serikali.
Mhe. Rais Magufuli amewataka Mawaziri kuandika maelezo yenye majibu ya changamoto na maoni hayo na kuwasilisha kwa Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa ndani ya kipindi cha wiki moja ili Serikali ifanyie kazi na kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji hapa nchini.
Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wafanyabiashara hao kwa mchango mkubwa wanaoutoa katika uchumi wa nchi na amewahakikishia kuwa Serikali itaendelea kuwapa ushirikiano wowote watakaouhitaji hususani katika ujenzi wa viwanda.
“Nataka kuwaambia kwa dhati kabisa, Serikali ninayoiongoza haiwachukii wafanyabiashara, inawapenda na itawaunga mkono, kama nilivyowaambia huko nyuma huu ndio wakati wenu wa kufanya biashara, fanyeni biashara zenu na lipeni kodi, hizi changamoto tumezipokea na tutazifanyia kazi” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa wafanyabiashara hao kuhakikisha wanashiriki katika miradi mikubwa anayotekelezwa na Serikali ikiwemo ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge), mradi wa umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stieglers’ Gorge), mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta la kutoka Hoima - Uganda hadi bandari ya Tanga - Tanzania, na amewataka wafanyabiashara wanaofanya vitendo vya udanganyifu katika kodi na uingizaji wa bidhaa wabadilike.
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa maelekezo yake ya kutaka utozaji wa kodi uangaliwe ili usiathiri shughuli za uwekezaji na uzalishaji, na amewataka wafanyabiashara kuendelea kufanya shughuli zao kwa amani kwa kuwa Serikali itaendelea kuwalinda.
Mapema Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) Dkt. Reginald Mengi amepongeza juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali kuimarisha uwekezaji zikiwemo kuimarishwa kwa sekta ya fedha, usimamizi mzuri wa uchumi na kuongezeka kwa mikopo.
Dkt. Mengi ametoa mapendekezo ya sekta binafsi yakiwemo kuiwezesha zaidi sekta binafsi ili iongeze uzalishaji na ulipaji wa kodi, kuweka vivutio vya kodi katika viwanda, kuimarisha miundombinu na vivutio vya kilimo, kupunguza urasimu katika uwekezaji, kuwepo mifumo ya kisasa ya ukusanyaji wa kodi na kuboresha utendaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
19 Machi, 2018
Hakimiliki ©2023 Habari - MAELEZO