JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
Dodoma, April 12, 2018:
SIKU moja baada ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad kuwasilisha taarifa yake Bungeni na kisha kuongea na waandishi wa habari, Serikali ya Awamu ya Tano imeonesha utendaji wa tofauti katika kutekeleza na kufanyiakazi hoja za ukaguzi.
Mawaziri wote ambao wizara zao zimeguswa na hoja mbalimbali za ukaguzi, pamoja na kuchukua hatua za haraka na kuwasilisha majibu rasmi Bungeni, kuanzia leo wataeleza kwa umma kupitia waandishi wa habari hatua walizozichukua za kufanyiakazi hoja husika.
Wakizungumza na waandishi wa habari leo mjini hapa, Dkt. Phillip Mpango, Waziri wa Fedha na Mipango, na Selemani Jafo, Waziri wa Nchi (Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa), wakifungua mfululizo wa mikutano hiyo, wamesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli, haitaruhusu fedha za umma zifanyiwe israfu.
Mawaziri hao wameipongeza Ofisi ya CAG kwa kazi nzuri kwani taarifa zake za ukaguzi zinasaidia lengo pana la Serikali ya Awamu ya Tano la kuhakikisha kila fedha inayokusudiwa kuwasaidia wananchi, inatumika ipasavyo ili kuyabadili maisha yao.
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali na hatua zinazochukuliwa na Serikali kutokana na ushauri uliotolewa katika ripoti hiyo, Wakati wa Mkutano Uliofanyika Leo Mjini Dodoma.
Dkt. Mpango: Tumerejesha Bilion 5 Zilizofujwa
Akijibu utekelezaji wa hoja ya kuwepo mafuta yaliyosamehewa kodi ya Shilingi bilioni 11.05 lakini yalitumiwa na makampuni yasiyostahili, Dkt. Mpango amesisitiza kuwa Serikali imefuatilia na kubaini hoja hiyo ni ya kweli. “Tayari Serikali imechukua hatua na kiasi cha Shilingi bilioni 5.53. Juhudi za kukusanya kiasi kilichobaki cha Shilingi bilioni 5.47 zinaendelea,” alisema.
Kuhusu hoja ya ongezeko la deni la matibabu nje ya nchi la shilingi bilioni 17.13, Waziri Mpango alisema deni hilo lilikua kutokana na wagonjwa wanaolazimika kusaidiwa matibabu ya muda mrefu nje ya nchi hasa saratani, kupandikizwa figo, mishipa ya fahamu, baadhi ya mahitaji ya upasuaji wa mifupa, moyo na baadhi ya magonjwa ya watoto.
Akifafanua hatua zilizochukuliwa kupunguza matumizi hayo miaka ijayo, Dkt. Mpango anasema kwa miaka ijayo mkakati wa Serikali ni kuhakikisha tiba hizo zinapatikana hapa nchini na tayari mafanikio yamepatikana.
“Hospitali ya Muhimbili imeshaanza kupandikiza figo; hospitali ya Jakaya Kikwete inafanya upasuaji wa moyo; Hospitali ya Ocean Road inakamilisha kufunga mashine za kisasa, Hospitali ya Mloganzila ina vifaa vyote na tutaajiri wataalamu wa kutosha; Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dodoma inakamilisha ufungaji vifaa vya kisasa, kuajiri mabigwa na imeshafanya upasuaji wa kwanza wa kupandikiza figo Machi, 2018,” alisema.
Kuhusu upungufu katika usimamizi wa fedha kwa mwaka 2016/2017, ambapo CAG amebaini ubadhirifu wa Shilingi milioni 332.86 katika Ubalozi wa Tanzania, Maputo, Msumbiji, Dkt. Mpango amesisitiza kuwa tayari mtumishi anayehusika amerejeshwa nyumbani na atafikishwa mahakamani.
Waziri Jafo: Watumishi 434 Wamebanwa
Akizungumzia hatua mbalimbali zilizochukuliwa katika sekta zake, Waziri Jafo amewaeleza waandishi wa habari kuwa CAG kubaini vitabu 379 vya kukusanya mapato ndio havikuwasilishwa ni mafanikio kwani katika ukaguzi wa mwaka uliopita, idadi hiyo ilikuwa kubwa zaidi ikiwa ni vitabu 871. Alisema mfumo mpya wa kukusanya mapato kielektroniki utakomesha kabisa tatizo hilo.
Hata hivyo, Waziri Jafo amesisitiza kuwa kutokana na kasoro hiyo na nyingine za udhaifu na uzembe wa baadhi ya watendaji, Serikali haitafumbia macho hali hiyo. “Jumla ya watumishi 434 wamechukuliwa hatua mbalimbali za kinidhamu na kisheria baada ya kubainika kuwa wamezisababishia Halmashauri zao hasara au hoja za ukaguzi zisizo za lazima.” alisema.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo akieleza kwa waandishi wa habari leo mjini Dodoma kuhusu hatua zilizochukuliwa na Serikali na zinazoendelea kuchukuliwa kutokana na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali na hatua zinazochukuliwa na Serikali kutokana na ushauri uliotolewa katika ripoti hiyo akiwemo kuwafikisha watendaji waliofanya ubadhilifu wa fedha za umma kwa mujibu wa ripoti ya CAG.
Alizitaja hatua hizo na takwimu zake kuwa ni: watumishi tisa (9) wamefukuzwa kazi, watumishi 210 wamepewa barua za onyo, watumishi 15 wamefikishwa kwenye vyombo vya dola na watumishi 28 wamesimamishwa kazi.
Aidha, watumishi wengine 13 wametakiwa kufidia hasara walizozisababisha kutoka kwenye mishahara yao, watumishi wanne (4) wameshushwa vyeo, watumishi 10 wamebadilishwa majukumu, na watumishi 64 wapo katika mchakato wa hatua za kinidhamu.
Katika mfululizo wa mikutano hiyo kesho Dkt. Harrison Mwakyembe, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Mhe. Charles Mwijage, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, watazungumza na waandishi wa habari saa 5:00 asubuhi kwenye ukumbi wa Idara ya Habari Bungeni.
Imetolewa na:
Dkt. Hassan Abbasi,
Mkurugenzi, Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali.
Hakimiliki ©2023 Habari - MAELEZO