Na: Lilian Lundo – MAELEZO, Arusha.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Selemani Jafo ametoa agizo kwa Ofisi za Mikoa na Halmashauri zote nchini kutenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa kwa vitengo vya Mawasiliano ili viweze kutekeleza majukumu yake.
Mhe. Jafo ametoa agizo hilo Jijini Arusha alipokuwa akifunga Kikao Kazi cha 14 cha Maafisa Mawasiliano Serikalini uliohudhuriwa na Maafisa Mawasiliano 300 kutoka katika Taasisi, Idara na Wakala wa Serikali, Mikoa, Majiji, Miji na Halmashauri zote nchini.
“Kuanzia mwaka ujao wa bajeti Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi wa Halmashauri, Majiji, Manispaa na Miji waweke kipaumbele kwa kutenga fedha za kununua vifaa muhimu kwa ajili ya Maafisa Habari na Mawasiliano ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo,” alisema Mhe. Jafo.
Vile vile ameagiza Maafisa Habari wapewe ushirikiano wa kutosha na Wakuu wa Idara kwa kuwapa taarifa na takwimu za idara zao ili kuwawezesha Maafisa hao kutoa taarifa muhimu za Serikali kwa vyombo vya habari na wananchi kwa wakati na bila vikwazo.
Aidha, amewataka Viongozi wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa kutambuua kuwa Afisa Habari ndiye Mtendaji Mkuu katika masuala ya uandaaji wa habari, hivyo ni muhimu Maafisa hao kuingia katika vikao mbalimbali ili wapate uelewa wa masuala mbalimbali ya kimaamuzi yanayofanywa na uongozi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Susan Mlawi amesema mada mbalimbali zimetolewa kwa lengo la kuwajengea uwezo Maafisa hao, ambapo miongoni mwa mada hizo ni pamoja na umuhimu wa Mawasiliano ya kimkakati katika kuisemea Serikali na tathmini ya utendaji katika mwaka 2017, maadili ya usalama katika kazi ya kuitangaza na kuisemea Serikali pamoja na wajibu wa Maafisa Habari katika mkakati wa kitaifa wa kupambana na maafa.
Nae, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo amesema ofisi yake itashirikiana na Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo kuhakikisha maazimio yote yaliyoafikiwa katika mkutano huo yanatekelezwa katika vitengo vyote vya Mawasiliano vya Halmashauri zote za Mkoa wa Arusha.
Mkutano wa Maafisa Mawasiliano Serikalini unafanyika kila mwaka, ambapo kwa mwaka huu unafanyika kwa mara ya 14. Mkutano huo umeandaliwa na Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Chama cha Maafisa Mawasiliano
Hakimiliki ©2023 Habari - MAELEZO