Na Mwandishi Wetu-Ofisi ya Waziri Mkuu
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameagiza kila kiwanda kilichopo nchini kihakikishe kinatumia alama za utambuzi za GS1 Tanzania simbomilia (barcodes).
Ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Februari 22, 2018) wakati akifungua Mkutano wa Sita wa Wamiliki wa Viwanda na Watumiaji wa simbomilia (barcodes). Hadi sasa GS1 ina wanachama 2000.
“Natoa wito kwa wenye viwanda kutumia GS1 Tanzania kutangaza na kuuza bidhaa zenye ubora katika maduka ya kimataifa, ambapo pia bidhaa zao zitachangia katika ulipaji wa kodi kwa usahihi”.
Amesema matumizi ya alama hiyo, iwe ndio chanzo cha kulipeleka Taifa kwenye kampeni ya kuhamasisha jamii kununua bidhaa zilizotengenezwa nchini. Hadi sasa
Waziri Mkuu amesema kama kila bidhaa itakuwa na utambuzi wa Taifa kiambishi “620”, wataweza kuwa na takwimu sahihi za wazalishaji ambao wanatambulika.
Pia Waziri Mkuu amesema utambuzi wa bidhaa zinazozalishwa nchini ukifanyika kwa kutumia GS1 kila duka litalipa kodi kwa kila bidhaa inayouzwa.
Hata hivyo Waziri Mkuu amesema barcodes ni muhimu kwa sababu zinawawezesha wajasiriamali kuuza bidhaa zao katika maduka rasmi ya nje na ndani ya Tanzania.
Amesema miaka ya nyuma kabla ya kuanzishwa kwa GS1 Tanzania, wazalishaji wa bidhaa za Tanzania walilazimika kwenda nje ya nchi yetu kutafuta barcodes ili waweze kuuza bidhaa zao
Waziri Mkuu amesema hali hiyo iliifanya Tanzania kuwa wategemezi na kuchangia kuzalisha ajira kwa ajili ya nchi nyingine kwa kununua barcodes zao. “Tangu kuanzishwa kwa chombo chetu, tumejinasua kutoka katika utegemezi huo.
Pia Waziri Mkuu amesema amefurahishwa na mipango iliyowekwa na GS1 Tanzania ya kuhakikisha kwamba mazao ya kilimo yanapatiwa barcodes na kuwaelimisha wananchi kuhusu alama hizo.
Mkutano huo umehudhuriwa na Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhandisi Stella Manyanya, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara SMZ, Balozi Amina Salum Ally, Katibu Mkuu, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Elisante Ole Gabriel.
Wengine ni Mwenyekiti wa Bodi ya GS1 Tanzania Dkt. Gidion Mazara, Wakuu wa Taasisi na Wadau wa GS1 kutoka Tanzania Bara na Visiwani (TBS, BRELA, TANTRADE, ZNCIAAL, COSTECH na Mtendaji Mkuu wa GS1 Tanzania Bi. Fatuma Kange.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, FEBRUARI 22, 2018.
Hakimiliki ©2023 Habari - MAELEZO