Na Mwandishi Wetu
Hatua za serikali kuhakikisha Watanzania wananufaika na rasilimali za nchi yao na kuongeza mapato zimeanza kuzaa matunda licha ya kupingwa vikali hapo awali.
Akiongea na waandishi wa habari leo Jijini Dar-es-Salaam, Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi, amesema hatua zilizochukuliwa kwenye sekta ya madini na kuboresha mifumo ya kukusanya mapato ya serikali imechangia kuongeza mapato maradufu.
Akieleza hatua zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano, Dkt. Abbasi amesema ni pamoja na ujenzi wa ukuta kwenye eneo la migodi ya madini ya Tanzanite Mirerani, kuanzishwa kwa masoko ya madini kwenye mikoa na wilaya nchi nzima na kuundwa kwa mifumo ya kisasa ya kijiditali ya kurekodi mapato ambayo licha ya kuongeza mapato, lakini pia imeongeza ufanisi.
Dkt. Abbasi amesema kuwa hadi kufikia mwezi Mei 2019 sekta ya madini kwa kipindi cha miezi kumi na moja ya mwaka wa fedha 2018/19 mapato yamefikia Shilingi bilioni 302.63 kiasi ambacho ni zaidi ya mapato yote kiasi cha Shilingi bilioni 301.6 yaliyopatikana kwenye mwaka wa fedha 2017/18.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Dkt. Abbasi mapato kwenye sekta ya madini katika kipindi cha miaka minne yamekuwa yakiongezeka mfululizo, akitolea mfano amesema mwaka 2016/17 makusanyo ya maduhuli yalikuwa bilioni 214.5 wakati mwaka 2015/16 maduhuli yalikuwa Shilingi Bilioni 210 na mapatao ya mwaka 2017/18 yalikuwa Shilingi bilioni 301.6
Aidha, aliongeza kuwa mapato yanayotokana na mauzo ya madini ya Tanzanite tangu ujenzi wa ukuta wa Mirerani ujengwe kuzunguka migodi ya madini hayo mapato yameongezeka maradufu kutoka kiasi cha shilingi milioni 71.8 mwaka 2015 hadi kufikia bilioni 1.43 mwaka 2017.
Akieleza mafanikio yaliyopatikana kutokana na uboreshaji wa mifumo ya kukusanya mapato Dkt. Abbasi amesema mifumo hiyo sio tu imeongeza mapato, lakini pia imeongeza ufanisi.
“Kabla ya Mfumo wa TTMS Serikali ilikuwa haipati kitu kabisa katika miito ya simu za nje wala kuwa na uwezo wa kuhakiki mapato ya simu za ndani lakini tangu mfumo huo ulipofungwa kwa eneo la mapato ya simu za nje tu Serikali imekwisha kusanya Shilingi bilioni 97.16 ikiwa ni malipo ya kodi zitokanazo na mapato ya kampuni za simu kwa simu kimataifa zinazoingia na kuishia hapa nchini” alifafanua Dkt. Abbasi.
Kuhusu ziara ya Rais Magufuli kwenye nchi za Afrika Kusini, Namibia na Zimbabwe Dkt. Abbasi ameeleza ziara hiyo licha ya kuwa na lengo la kuimarisha ushirikiano wa kihistoria, lakini pia ilikuwa na lengo la kutafuta fursa za kibiashara. “Kwenye ziara hiyo Rais Magufuli ameweza kufikia makubaliano ya kuongeza kiwango cha biashara na uwekezaji kwenye sekta ya utalii, usafiri wa anga na miundombinu pia Tanzania imeweza kupata soko la mahindi tani 700,000 nchini Zimbabwe”.
Aidha, Dkt. Abbasi amewasihi Watanzania wenye ujuzi wa kufundisha Lugha ya Kiswahili kuitumia vyema fursa ya kufundisha lugha hiyo nchini Afrika Kusini kwa kujisajili kwenye kanzi data ya wataalamu wa Kiswahili Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) ili wapate ithibati na kutambulika rasmi.
Kuhusu ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo, Msemaji Mkuu wa Serikali amewahakikishia Watanzania majadiliano juu ya mrad huo bado yanaendelea na Serikali ya Awamu ya Tano itahakikisha maslahi ya nchi yanawekwa mbele ili wanufaike na rasilimali za nchi yao.
Mkutano wa Msemaji Mkuu wa Serikali na vyombo vya habari umelenga kueleza utekelezaji wa serikali katika sekta mbalimbali ikiwemo madini, miundombinu, mawsiliano na sekta nyingine.
Hakimiliki ©2023 Habari - MAELEZO