RAIS Dkt. John Magufuli ameihakikishia Serikali ya Jamhuri ya Kiarabu ya Misri na wadau wa maendeleo kuwa Serikali yake itasimamia utekelezaji wa mradi wa kuzalisha umeme katika Mto Rufiji (Stiegler’s Gorge) kwa kuwa ndiyo njia sahihi ya kufikia Uchumi wa Viwanda ifikapo mwaka 2025.
Akizungumza katika Hafla ya Utiaji saini ya Mkataba wa Ujenzi wa Mradi huo leo Jumatano (Desemba 12,2018) Jijini Dar es Salaam na kushuhudiwa na Waziri Mkuu wa Misri, Dkt. Mostafa Madbouly, Rais Magufuli alisema Serikali ya Awamu ya Tano ipo imara na itahakikisha kuwa mradi huo utakaozalisha Megawati 2100 unakamilika kwa wakati ili kuiwezesha Tanzania kuweza kupiga hatua kubwa zaidi katika maendeleo.
Rais Magufuli alisema Serikali ya Awamu ya Tano imekusudia kuharakisha utekelezaji wa mradi wa umeme wa Mto Rufiji Stiegler’s Gorge huo kutokana na ukweli kuwa uzalishaji wa umeme kwa chanzo cha maji ni rahisi katika uzalishaji wake ukilinganisha na vyanzo vingine vya uzalishaji wa nishati ya umeme ikiwemo upepo, makaa ya mawe, nyuklia, jua na joto ardhi.
“Ukiutazama mradi huu wa Stiegler’s Gorge unatoka katika mikoa na maeneo ambayo yana kiasi kikubwa cha mvua, lakini pia umeme wa maji ni rahisi sana ni Tsh 36 kwa uniti moja ukilinganisha na Nyuklia (Tsh 65), Jua (Tsh 103.5), joto ardhi (Tsh 114.5), upepo (Tsh 103.5), Makaa ya Mawe (Tsh 118), na mradi huu ukikamilika bei ya umeme itashuka kwa kiasi kikubwa sana” alisema Rais Magufuli.
Aidha Rais Magufuli alisema kukamilika kwa utekelezaji wa mradi wa ujenzi huo, kutaiwezesha Tanzania kuzalisha kiasi kikubwa cha umeme kitachokasaidia kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa uchumi wa viwanda na mradi wa reli ya kisasa, hatua itakayoiwezesha kupiga hatua kubwa za maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wake.
Akifafanua zaidi Rais Magufuli alisema kabla ya kufikiwa kwa uamuzi wa utekelezaji wa mradi huo, kulitokea baadhi ya makundi ya watu waliokuwa wakipinga kujengwa kwa mradi huo huo kwa kigezo kuwa mradi huo utaleta tishio la uharibifu wa mazingira katika hifadhi ya selous jambo ambalo halina ukweli wowote.
“Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Timu ya Watalaamu wa Serikali, hakutokuwa na athari yoyote ya mazingira na kwa kuwa mradi wote unachukua aslimia 1.8 ya eneo la hifadhi, lakini eneo lile litakuwa eneo mahsusi kwa wanyama, ndege na viumbe wote wa majini ikiwemo kuongezeka kwa mazalia ya samaki” alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli alisema mradi huo unajengwa na mkandarasi wa kampuni ya Arab Contractor utagharimu kiasi cha Trilioni 6.5 unatarajiwa kujengwa kwa kipindi cha miezi 42 ambapo Serikali imetoa sita kati ya miezi 36 ya ukamilishaji wa mradi huo, kwa mkandarasi kuweza kukusanya vifaa vyake na kuvipeleka katika eneo la mradi.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Misri Dkt. Mostafa Madbouly alisema Serikali yake itaendelea kuimarisha ushirikiano wa kiufundi, kitaalamu na kidiplomasia na Tanzania ili kuhakikisha kuwa ndoto za waasisi wa urafiki wa mataifa hayo zinaweza kutimizwa ikiwemo utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Aliongeza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Kiarabu ya Misri imeridhishwa na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano kupitia kwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo iliyofikiwa na Tanzania katika kipindi kifupi cha utawala tangu kuingia kwake madarakani mwaka 2015.
Kwa mujibu wa Madbouly alisema katika kipindi cha miaka michache ijayo, Serikali ya Misri kupitia kwa taasisi zake za kiuchumi zitaendelea kuwekeza kwa kasi zaidi nchini Tanzania ili kuhakikisha kuwa miradi yote ya maendeleo inayotekelezwa na Tanzania inaweza kuleta tija kwa wananchi wake.
Awali akitoa taarifa ya mradi huo, Waziri wa Nishati wa Tanzania, Dkt. Medard Kalemani alisema Mradi wa Stiegler’s Gorge ni moja ya miradi mikubwa ya kufua umeme katika dunia na Afrika kwa ujumla na hivyo utekelezaji wake utaiweka Tanzania katika ramani ya juu zaidi ulimwenguni.
Dkt. Kalemani alisema kupitia katika vyanzo mbalimbali vya nishati ya umeme vilivyopo nchini, Serikali ya Awamu ya Tano imekusudia kuhakikisha Tanzania inaweza kuzalisha Megawati 5000 za umeme ifikapo mwaka 2020 na Megawati 10,000 ifikapo mwaka 2025 na hivyo kuiwezesha Nchi kuwa muuzaji wa umeme katika nchi jirani.
“Tumepanga kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2025, tunakuwa na umeme katika kila kijiji na hili litawezekana kwa kupitia utekelezaji wa miradi ya umeme iliyopo nchini, na mradi wa Mto Rufiji ni mojawapo ya vipaumbele vya kimkakati” alisema Dkt. Kalemani.
Hakimiliki ©2023 Habari - MAELEZO