Na Beatrice Lyimo-MAELEZO, Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ametangaza rasmi kwa mamlaka aliyonayo kuipandisha hadhi Manispaa ya Dodoma kuwa Jiji.
Dkt. Magufuli ameyasema hayo leo Mkoani Dodoma wakati wa Maadhimisho ya Miaka 54 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaliyoadhimishwa Uwanja wa Jamhuri mkoani humo.
“Tuliona Dar es Salaam ilivyokuwa makao makuu kipindi hicho na ilikuwa inaitwa Jiji, nikaona niangalie katika nchi yetu kuna Majiji mangapi, tuna Manispaa ngapi, Halmashauri ngapi na mimi nina mamlaka gani katika kutengeneza Majiji au Manispaa, nikakuta Dar es Salaam ni Jiji, Tanga ni Jiji, Arusha ni Jiji, Mwanza ni Jiji, Mbeya ni Jiji nikaambiwa Dodoma ni Manispaa nikasema hili haliwezekani kwa hiyo kuanzia leo kwa mamlaka waliyonipa Watanzania Dodoma ni Jiji”
“Kwa hiyo maandalizi yote ya kisheria lazima yaanze sasa kufanyika na huyu Mkurugenzi aliyekuwa wa Manispaa hapa hapa leo anakuwa Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma na hili litakuwa Jiji la peke yake kwa sababu lipo katikati ya Tanzania” ameongeza Dkt. Magufuli.
Aidha, Dkt. Magufuli amesema kuwa anatarajia kufanya mazungumzo na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Dkt. Akinwumi Ayodeji Adesina ambao wanafadhili miradi 25 hapa nchini yenye thamani ya Dola Bilioni 1.986, ili kati ya miradi mbalimbali atakayoongea, Dodoma ipewa kipaumbele kama Jiji.
Akizungumzia kuhusu miaka 54 ya Muungano Rais Magufuli amesema kuwa, Tanzania imekuwa na mafanikio mbalimbali ikiwemo kuongezeka kwa maeneo ya ushirikiano, ambapo mwaka 1964 yalikuwa maeneo 11 na sasa yapo maeneo 22, Muungano umefanya nchi imekuwa na sauti na kujiamini, vile vile kutoa mchango katika masuala mbalimbali ya Kimataifa na kusuluhisha migogoro.
Mbali na hayo Rais Magufuli amewataka Wananchi kulinda na kuudumisha Muungano uliopo na kutoa ushiririkiano kwa vyombo vya usalama kwani Muungano huo ni tunu kwa Taifa.
“Kikubwa kwa Watanzania bila kujali dini, kabila, vyama tusimame imara, tutunze na kuusimamia huu Muungano kwa nguvu zetu zote, Serikali ninayoiongoza na Serikali ya Zanzibar tupo imara, Muungano huu tutaulinda kwa nguvu zote, tutautunza na kuusimamia” amesisitiza Dkt. Magufuli.
Tanzania imeadhimisha Sherehe za miaka 54 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibari ambapo Maadhimisho hayo yamebeba kauli mbiu isemayo “Muungano wetu ni wa mfano Duniani tuuenzi, tuulinde, tuuimarishe na kuudumisha kwa maendeleo ya Taifa letu”
Hakimiliki ©2023 Habari - MAELEZO