Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 09 Julai, 2019 amezindua Hifadhi ya Taifa ya Burigi-Chato iliyoundwa baada ya kuunganishwa kwa Mapori ya Akiba ya Burigi, Biharamulo na Kimisi yaliyopo katika Wilaya za Biharamulo, Ngara, Karagwe na Muleba Mkoani Kagera na Chato Mkoani Geita.
Hifadhi hiyo inakuwa ni ya 3 kwa ukubwa hapa nchini ikiwa na jumla ya kilometa za mraba 4,702, ikitanguliwa na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha (kilometa za mraba 20,300) na Serengeti (kilometa za mraba 14,763).
Sherehe za uzinduzi wa hifadhi hiyo zimefanyika katika Kijiji cha Katete, Wilaya ya Chato Mkoani Geita na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mawaziri na Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Mabalozi wanaoziwakilisha nchi mbalimbali hapa nchini, Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Viongozi wa Dini, Viongozi wa vyama vya siasa na viongozi wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
Kabla ya kuzindua hifadhi hiyo Mhe. Rais Magufuli amekagua gwaride la Jeshi Usu la Wanyamapori na Misitu, ameshuhudia Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamis Kigwangallah akiwavalisha vyeo Makamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), amepokea tuzo ya Hifadhi ya Serengeti iliyopata ushindi wa kuwa hifadhi bora Barani Afrika kwa mwaka 2019 na tuzo ya Mlima Kilimanjaro ulioshinda kwa kuwa kivutio bora Barani Afrika kwa mwaka 2017 na pia amekabidhi vyeti kwa wawekezaji 6 waliotayari kuwekeza katika Hifadhi ya Taifa ya Burigi-Chato.
Kabla ya hotuba yake, Mhe. Rais Magufuli aliwataka wote walioshiriki uzinduzi wa hifadhi hiyo kusimama kwa dakika 1 kwa ajili ya kuwakumbuka watu 7 wakiwemo wafanyakazi 5 wa kituo cha Televisheni cha Azam TV waliopoteza Maisha katika ajali ya barabarani iliyotokea jana asubuhi kati ya Igunga (Tabora) na Shelui (Singida) baada ya basi walilokuwa wakisafiria kuja kurusha matangazo ya uzinduzi huo kugongana uso kwa uso la lori la mizigo.
Katika hotuba yake, Mhe. Rais Magufuli ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii na wadau mbalimbali kwa juhudi kubwa zilizofanyika katika uhifadhi wa maliasili ikiwemo hifadhi za wanyamapori hali iliyowezesha uoto wa asili kurejea na idadi ya Wanyama kuongezeka, wakiwemo Tembo ambao wameongezeka kutoka 43,330 mwaka 2014 hadi zaidi ya 60,000 na Faru ambao wameongezeka kutoka 15 hadi kufikia 167 hivi sasa.
Mhe. Rais Magufuli amesema kuanzishwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Burigi- Chato kulikotanguliwa na kutangazwa kwa Pori la Akiba la Ibanda kuwa Hifadhi ya Taifa ya Ibanda-Kyerwa na Pori la Akiba la Rumanyika-Orugundu kuwa Hifadhi ya Taifa ya Rumanyika-Karagwe ni juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano za kuendeleza sekta ya uhifadhi na utalii ambapo sasa Tanzania inakuwa na eneo la hifadhi lenye jumla ya kilometa za mraba 361,594 sawa na asilimia 32 ya eneo la nchi nzima na hivyo kuwa nchi yenye eneo kubwa lililohifadhiwa kuzizidi hata nchi ambazo ni kubwa zaidi ya Tanzania kwa eneo Barani Afrika.
Mhe. Rais Magufuli amesema pamoja na juhudi mbalimbali zilizofanywa kuhifadhi maliasili hapa nchini zikiwemo kuanzishwa hifadhi mpya, kutekeleza mkakati wa kuendeleza utalii katika Kanda ya Kusini kwa gharama ya shilingi Bilioni 340 na kuongeza mapambano dhidi ya ujangili, Serikali imechukua hatua nyingine madhubuti za kukuza utalii na uhifadhi zikiwemo kujenga na kuboresha viwanja vya ndege 11 hapa nchini, kununua ndege 8 ambapo 6 zimeshawasili na kuanza kutoa huduma za usafiri wa anga na kutekeleza mradi mkubwa wa katika mto Rufiji ambao utazalisha megawati 2,115 za umeme zitakazosaidia kupunguza matumizi makubwa ya kuni na mkaa ambao husababisha ekari 400,000 za miti kukatwa kila mwaka.
Ameongeza kuwa hatua hizo zimeanza kuzaa matunda kwani idadi ya watalii wanaotembelea hapa nchini imeanza kuongezeka kutoka watalii 1,100,000 mwaka 2015 hadi kufikia watalii 1,500,000 mwaka 2018 na kwamba yapo matumaini makubwa ya kufikia malengo ya watalii 2,000,000 mwaka 2020.
Mhe. Rais Magufuli ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kuongeza juhudi za kuwavutia watalii zaidi zikiwemo kupunguza gharama za utalii, kuboresha hoteli za watalii, kupanua vivutio na huduma kwa watalii na kuwa na watoa huduma za utalii wazuri.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kuwapa motisha wote wanaofanya kazi nzuri za uhifadhi na kukuza utalii hapa nchini, na katika hilo amemtaka Waziri Dkt. Kigwangallah kuwapa zawadi viongozi walioshiriki katika operesheni ya kuwaondoa wavamizi na wafugaji waliokuwa wameingiza mifugo katika Pori la Akiba la Burigi wakiongozwa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jen. Mstaafu Salum Kijuu ambaye amezawadiwa shilingi Milioni 10 na Cheti, Wakuu wa Wilaya Shilingi Milioni 5 na Cheti kila mmoja na viongozi wengine waliopatiwa shilingi Milioni 2 na Cheti.
“Mimi nafahamu jinsi Meja Jen. Mstaafu Kijuu alivyofanya kazi kubwa ya kusafisha pori hili lilipovamiwa na wafugaji, nilimpa siku 3 awe ameondoa mifugo yote na kweli ndani ya siku 3 mifugo iliondoka na matokeo yake leo tuweza kuanzisha Hifadhi ya Taifa hapa, kabla yake ilikuwa haiwezekani, nakupongeza sana Meja Jen. Mstaafu Kijuu, Wakuu wa Wilaya na wote walioshiriki katika operesheni ile” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Kuhusu zawadi ya sanamu ya Baba wa Taifa aliyopewa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kutambua mchango wake wa kuyaenzi maono ya Baba wa Taifa, Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere, Mhe. Rais Magufuli ameshukuru kwa zawadi hiyo na ameagiza wizara ijenge jengo litakalohifadhi sanamu hiyo ndani ya hifadhi ya Burigi- Chato na jengo hilo liitwe Kambi ya Kijuu (Kijuu Camp).
Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa Mabalozi na wawekezaji mbalimbali wa ndani na nje ya nchi kujitokeza kuwekeza katika maeneo ya hifadhi ambayo kwa sasa yana fursa nyingi na pia ametoa wito kwa Watanzania kuhakikisha wananufaika na kuinuka kwa utalii hapa nchini.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamis Kigwangallah amesema kuanzishwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Burigi-Chato kunafanya idadi ya Hifadhi za Taifa kuongezeka kutoka 16 hadi 19 na kwamba wizara hiyo inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha huduma kwa watalii ikiwemo kujenga hoteli 3 za nyota 3 katika maeneo ya hifadhi, hosteli, kujenga gati za maboti ya watalii, barabara na viwanja vya michezo katika hifadhi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chato
09 Julai, 2019
Hakimiliki ©2023 Habari - MAELEZO