Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye pamoja na Naibu Waziri wa Utamaduni kutoka Jamhuri ya watu wa China Mhe. DONG WEI wamesaini programu ya utekelezaji wa Mkataba wa masuala ya Utamaduni wa miaka mitatu kuanzia mwaka 2017 hadi 2020 leo Jijini Dar es Salaam.
Waziri Nape ameeleza kuwa Mkataba huo unalengo la kuimarisha na kuendeleza ushirikiano katika Sekta ya Utamaduni ambao umedumu kwa miaka mingi ulioasisiwa na Baba wa Taifa Mwl.Julius K. Nyerere.
“Tanzania na China tumekuwa na ushirikiano wa muda mrefu wa masuala mbalimbali ikiwemo hili la Utamaduni ambalo limetumika kukuza, kulinda na kuunganisha nchi zetu kuwa kitu kimoja”, Alisema Mhe. Waziri.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Utamaduni wa China Mhe. DONG WEI amesema kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na China uliokuwepo kwa muda mrefu katika masuala ya Utamaduni, Sanaa, Elimu,Ngoma na Michezo yamesaidia kuimarisha ushirikiano uliopo na kuwezesha nchi hizi mbili kunufaisha katika maeneo hayo.
“Ushirikiano wetu wa muda mrefu katika masuala ya Utamaduni umeleta mafanikio makubwa ambayo sote tunajivunia kila tunapokuwa pamoja”.Alisema Mhe. WEI.
Mkataba huo pamoja na mambo mengine una lengo la kuendeleza na kufanya mpango wa pamoja kwa siku za usoni, kufanya matokeo makubwa katika Sekta ya Utamaduni kati ya nchi hizo mbili, Kufanya mkutano maalum wa ushirikiano wakati muafaka, kuzidisha ushirikiano kwenye sekta ya viwanda katika bidhaa za Utamaduni na Kubadilishana wataalamu na mafunzo ya kiutamaduni.
Katika hatua nyingine Serikali hiyo ya China imeisaidia Wizara kiasi cha Yuan laki nne (400,000) kwa ajili ya kununua vifaa mbalimbali kwa ajili ya matumizi ya Wizara.
Hakimiliki ©2023 Habari - MAELEZO