Na: Lilian Lundo - MAELEZO, Dodoma.
Serikali inaendelea na mpango wa kuhamasisha ulimaji wa mazao makuu matano ya Pamba, Korosho, Tumbaku, Kahawa na Chai nchini ili kuongeza uzalishaji wa mazao hayo.
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa ameyasema hayo leo Bungeni Mjini Dodoma wakati wa maswali kwa Waziri Mkuu alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Sumve Mhe. Richard Ndassa juu ya namna Serikali ilivyojipanga na utafutaji wa masoko ya Pamba kutokana na mwitikio mkubwa wa kulima zao hilo mwaka huu.
"Miongoni mwa mikakati ya kuendeleza mazao hayo ni pamoja na kulima kisasa na kutafuta masoko ndani na nje ya nchi," alisema Waziri Mkuu.
Amesema, mwezi huu anatarajia kukutana na watumiaji wa zao la Pamba hapa nchini ili kuweka mfumo endelevu wa ununuzi wa zao hilo. Aidha, Wizara ya Kilimo inafanya kazi ya kutafuta masoko nje ya nchi.
Pia, Mhe. Majaliwa alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Liwale Mhe. Zuberi Kuchauka juu ugawaji wa pembejeo za korosho kwa mwaka huu amesema, Serikali ilitoa pembejeo ya Salfa bure mwaka jana kwa wakulima wa korosho ili kufanya hamasa kwa zao hilo baada ya wakulima kutelekeza zao hilo kutokana na kukosa pembejeo hiyo.
"Baada ya ugawaji wa pembejeo hiyo ya Salfa zao hilo limevunwa kwa kiwango cha juu kwa mwaka jana, hivyo kutokana na fedha walizozipata wakulima wa zao hilo watatatikiwa kuchangia gharama za Salfa kwa mwaka huu," alisema Mhe. Majaliwa.
Wakati huo huo, Mhe. Kassim Majaliwa alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Urambo Mhe. Margaret Sitta juu ya migogoro ya mipaka ya mapori na misitu, amesema Serikali imeiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kushirikisha wanavijiji na viongozi wa kijiji wakati wa uwekaji wa mipaka hiyo.
Hata hivyo amesema ikiwa kijiji kitaonekana kiko ndani ya mipaka ya msitu au pori, tathimini itafanyike na baadae watapewa elimu ya kutoingia ndani ya mipaka ya misitu na mapori ya Serikali Kuu
Misitu yote ya Serikali Kuu inahifadhiwa kisheria na mipaka hiyo inaonekana ili kuondoa migogoro na wananchi.
Hakimiliki ©2023 Habari - MAELEZO