Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewahakikishia Watanzania wote kuwa Taifa linakwenda katika mwelekeo mzuri hasa baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha uchumi na huduma za kijamii kama vile afya, elimu, maji, nishati na miundombinu ya usafiri.
Mhe. Rais Magufuli amesema hayo leo tarehe 05 Februari, 2019 alipokutana na wananchi katika Mtaa wa Zanaki, Wilaya ya Ilala Jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya kutembelea kampuni ya Africa Media Group (AMGL) yenye vituo vinne vya televisheni ikiwemo channel Ten na vituo viwili vya redio ikiwemo Magic FM, ambayo kwa sasa inamilikiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM).
Mhe. Rais Magufuli amesema pamoja na mafanikio hayo, Serikali itaendelea kupambana na dhuluma na matumizi mabaya ya rasilimali za Taifa na ametoa wito kwa Watanzania wote kuiunga mkono kwa kuhakikishia wanatanguliza maslahi ya Taifa.
Akiwa ndani ya jengo la AMGL, Mhe. Rais ambaye ni Mwenyekiti CCMamejionea mitambo, chumba cha habari na studio za kurushia matangazo za kituo cha redio cha Magic FM na kituo cha televisheni cha Channel Ten, na pia amezungumza na wafanyakazi ambao wamemueleza changamoto mbalimbali zikiwemo uhaba na uchakavu wa vitendea kazi, maslahi madogo ya wafanyakazi na uchakavu wa jengo la kituo hicho.
Mhe. Rais Magufuliameahidi kutoa shilingi Milioni 200 ndani ya siku 2 kwa ajili ya kununulia vitendea kazi vya kituo hicho na pia amewataka wafanyakazi wa AMGL kumpelekea mapendekezo ya jengo lolote la CCM lenye hadhi nzuri ili kuhamishiwa kituo hicho.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wafanyakazi hao kwa kazi nzuri wanazozifanya na amesema kuwa dhamira yake ni kuhakikisha kituo hicho kinaboreshwa, matangazo yake yanafika maeneo mengi ya ndani na nje ya nchi na kinakuwa kituo cha mfano kwa vituo vingine hapa nchini.
Pia amewataka wafanyakazi hao kujenga umoja wa dhati, kuchapa kazi kwa juhudi zaidi ili kuongeza uzalishaji wa mapato na kuzalisha maudhui ambayo yatawasaidia Watanzania kupata manufaa kama vile kutoa elimu ya kilimo, biashara, ufugaji na uvuvi.
“Nataka Africa Media Group Ltdiwe na vyombo vyenye nguvu, vinavyotazamwa kila mahali hapa nchini hadi nje ya nchi, Tanzania haiwezi kuwa soko la kuangalia vyombo vya habari vya kutoka nje ya nchi, watu waangalie vyombo vya habari vya nje lakini vyombo vyetu viwe ndio mwongozo wa maisha ya Watanzania zaidi ya Milioni 50.
“Na hii natoa wito kwa vyombo vyote vya Tanzania, mna wajibu wa kuzungumzia mazuri ya Tanzania, lakini pia muendelee kutoa elimu kwa Watanzania, Watanzania karibu asilimia 75 ni wakulima, toeni vipindi vya kuonesha kilimo bora, ufugaji bora, nakadhalika” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Baada ya kutoka AMGL, Mhe. Rais Magufuli amekagua mradi wa ukarabati mkubwa wa jengo la kitega uchumi la CCM(SUKITA) lililopo mtaa wa Lumumba Jijini Dar es Salaam ambalo litakamilika mwezi Juni mwaka huu, na akiwa nje ya jengo hilo amesalimiana na wananchi wakiwemo wafanyabiashara ndogondogo ambao amewahakikishia kuwa Serikali itaendelea kutimiza wajibu wake wa kuwapigania Watanzania wote bila kubagua.
Mhe. Rais Magufuli amemalizia ziara yake kwa kutembelea Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya CCM Lumumba Jijini Dar es Salaam na kuzungumza na wafanyakazi ambapo amewahakikishia kuwa chama chao (ambacho ni chama tawala) kinakwenda vizuri hasa baada ya hatua zilizochukuliwa kusimamia misingi ya chama, mali na mapato ya chama, maadili na uongozi na pia kurejesha mali za chama zilizokuwa mbioni kupotea.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
05 Februari, 2019
Hakimiliki ©2023 Habari - MAELEZO